Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umetekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 1.6 kwa gharama nafuu katika Kijiji cha Nangose, Kata ya Temeke, Halmashauri ya Mji wa Masasi ambazo hazikuwahi kujengwa tangu taifa lipate uhuru.
Mhe. Jenista amesema hayo wakati akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Nangose mara baada ya kukagua barabara hizo zilizojengwa na TASAF kupitia mradi wa ajira za muda.
Mhe. Jenista amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kujenga barabara zenye urefu wa Kilometa 1.6 katika Kijiji cha Nangose, ambapo tangu nchi ipate uhuru hakukuwa na barabara zaidi ya kuwepo na njia za miguu ambazo zilikuwa ni kikwazo cha kijiji hicho kupata maendeleo.
“Barabara hizi zimejengwa kupitia mradi wa ajira za muda kwa gharama nafuu sana ambayo ni kiasi cha shilingi milioni 3.6, ambapo fedha hiyo ililipwa kwa walengwa wa TASAF waliokuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara hizo,” Mhe. Mhagama amefafanua
.Katika kuhakikisha barabara hizo zinakuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi katika kijiji hicho, Mhe. Mhagama amemtaka Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji Masasi kuimarisha barabara hizo ili zitumike kwa muda mrefu na kuwa chachu ya maendeleo katika Kijiji cha Nangose.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Claudia Kitta amesema kuwa wananchi wa Kijiji cha Nangose ambao ni walengwa wa TASAF wamefanya kazi ya ujenzi wa barabara hizo zenye urefu wa kilomita 1.6 kupitia mradi wa ajira za muda, na kuongeza kuwa katika Halmashauri ya Mji Masasi zipo barabara 40 ambazo zimejengwa na TASAF kupitia mradi huo wa ajira za muda.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Nangose, Diwani wa Kata ya Temeke Mhe. Frank Malanjila amesema kabla ya TASAF kuwezesha ujenzi wa barabara katika kata yake, kulikuwa na changamoto kubwa lakini kwasasa barabara zilizojengwa zimeunganisha vijiji na kuwawezesha wananchi kutoka eneo moja kwenda jingine, ikiwa ni pamoja na kusafirisha bidhaa na mazao yao kwa urahisi tofauti na ilivyo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.