Baraza la Wazee Masasi limeshangazwa na ubora wa vifaa tiba na miundombinu inayopatikana katika vituo vya kutolea huduma za Afya mara baada ya kutembelea Hospitali ya Mkomaindo, Kituo cha Afya Mtandi na Kituo cha Afya Mbonde huku wakimpongeza Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe. Geoffrey Mwambe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko hayo ya kihistoria katika vituo vya kutolea huduma za Afya Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara.
Wamesema hayo Julai 15, 2024 katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe, Geoffrey Mwambe akiambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mhe. Hashim Namtumba, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya Mhe. Ally Salvatory, Mganga Mkuu Dkt. Salum Gembe na wataalamu mbalimbali aliyoiandaa mahususi kwa ajili ya Baraza la Wazee Masasi kutembelea vituo vya kutolea huduma za Afya.
Wakizungumza Katika ziara hiyo, wamesema mabadiliko waliyoyashuhudia ni yakistoria na kuwaomba wananchi wafike katika vituo vya kutolea huduma za Afya kujionea wenyewe maboresho hayo makubwa ambayo hajayawahi kutokea kwa miaka mingi.
“Kwakweli katika ziara hii, Nimefarijika sana kwa juhudi zake na usimamizi wake, Mhe. Geoffrey Mwambe, Wito wangu wananchi wengine waje Hospitali, ebu waje hospitali waone hospitali ilivyobora, ilivyokuwa na mambo ya kisasa na yakuridhisha na sisi Masasi tusiite masasi, napenda tuiite (New Masasi) kwa maana ya Masasi mpya, niwaombe wananchi wasiishie kusikia tu, waje wajionee wenyewe), Wamesema.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe Mwambe amesema mageuzi mbalimbali yamefanyika kuanzia majengo na vifaa tiba ili wananchi wa Masasi waweze kunufaika na huduma hizo.
“Mageuzi yamefanyika Mkomaindo na yanaendelea kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya, majengo tuliyojenga na huduma tunazotoa ziendane, Tubadilishe fikra ili kuleta imani kwa wananchi. Vituo vya afya Mtandi na Kituo cha Afya Mbonde tumevijenga kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Mkomaindo na ili tubadili fikra ni muhimu Madaktari kutoa huduma kwa wakati, tuimarishe upande wa kujifungua, tuimarishe Upatikanaji wa dawa hospitali sambamba na huduma za mionzi”. Amesema
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mhe. Hashim Namtumba amesema kazi kubwa imefanyika katika maboresho hayo kilichobaki ni kubadili fikra na mitazamo kwa wananchi ambao bado wanamitazamo hasi za huduma za miaka ya zamani.
Mganga Mkuu, Dkt. Salum Gembe amesema ataendelea kusimamia masuala ya afya kwa ukamilifu na uadilifu ili utoaji wa huduma za Afya uendelee kuwa bora na kwamba kupitia Mkurugenzi wa Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu wamejipanga kuhakikisha ubora na viwango vya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi unaimarika na kwamba wanatarajia kufunga kamera za CCTV hospitali ya Mkomaindo ili kutazama mienendo ya utoaji wa huduma.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.