Wataalamu wa Afya kutoka Halmashauri ya Mji Masasi wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Masasi Dkt. Salum Gembe wametoa elimu ya tahadhari juu ya ugonjwa wa Mpox katika Kanisa la Anglikana lililopo Mtaa wa Wapiwapi.
Ikumbukwe kuwa, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama March 15, 2025 aliwataka wataalamu wa afya Nchini kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu ya tahadhari juu ya ugonjwa huo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Masasi Dkt. Salum Gembe amesema kuwa ni vyema wakazi wa Masasi kuchukua tahadhari mapema ili kujikinga na ugonjwa huo kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Aidha Dkt. Gembe amewataka wananchi kutoa taarifa haraka wanapoona kuna mtu ana dalili za ugonjwa huo ili wataalamu wamfanyie vipimo na kudhibiti hatari zaidi kwa wengine.
Naye, Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji Masasi, Benjamin Shilinde akitoa elimu juu ya ugonjwa huo amesema kuwa dalili za ugonjwa wa Mpox ni kama vile kutoka vipele vikubwa usoni na sehemu zote za mwili na kuvimba mitoki ya mwili.
Pia ameweka wazi jinsi ugonjwa wa Mpox unavyoweza kuambukizwa kwa njia kama vile kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye maambukizi ya Mpox, kugusana na mtu mwenye dalili za Mpox, kugusa vitu vilivyotumiwa na mtu mwenye maambukizi ya Mpox na kula au kugusa mizoga au wanyama pori walioambukizwa mfano nyani, sokwe, tumbili au swala wa msituni.
Aidha alieleza namna ya kujikinga na ugonjwa wa Mpox kwa njia kama kuepuka kusogeleana karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, epuka kugusa vyombo, matandiko, nguo au godoro la mtu mwenye ugonjwa wa Mpox, epuka kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye Mpox, epuka kusalimiana kwa kukumbatiana, kubusiana au kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi ya Mpox, nawa mikono yako mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au tumia vitakasa mikono, vaa barakoa ikiwa unaongea na mtu mwenye dalili za Mpox, epuka kula au kugusa mizoga au wanyama pori wenye maambukizi, ziba mdomo kwa kiwiko unapokohoa au kupiga chafya, safisha na takasa sehemu zote na vitu ambavyo vinaguswa mara kwa mara, pia epuka kugusana na mtu mwenye dalili za Mpox.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.