Wananchi wa Halmashauri ya Mji Masasi wanakwenda kunufaika na ujenzi wa barabara ya Mnivata-Newala- Masasi yenye urefu wa kilometa 160 mara baada ya kukamilika kwa zoezi la Serikali kusaini mikataba miwili yenye gharama ya jumla ya Shilingi bilioni 234.512 inayokwenda kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji mkoani Mtwara.
Ujenzi wa barabara hiyo utaboresha mtandao wa barabara na madaraja kwa Ukanda wa kusini na hivyo kuboresha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa June 21, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe, Profesa Makame Mbarawa wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo katika hafla iliyofanyika viwanja vya Sabasaba wilayani Newala.
Profesa Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hiyo utaboresha usafiri na usafirishaji wa malighafi za viwandani kama vile makaa ya mawe na saruji, mazao ya chakula na kilimo, bidhaa za biashara na mazao ya misitu, mifugo na uvuvi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.., madhumuni ya ujenzi ujenzi wa barabara ya Mnivata-Newala- Masasi yenye urefu wa kilometa 160 ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kukuza uchumi wa wananchi, sasa mnakwenda kupata barabara bora na yenye viwango,” amesema Profesa Mbarawa
Mtendaji mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta amesema mikataba hiyo ni baina ya Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na kampuni ya China Wu Yi Co ltd itakayojenga barabara kutoka Mnivata-Mitesa (Km 100) kwa gharama ya Shilingi bilioni 141.964 na kampuni ya China Communications Construction Co. ltd itakayojenga sehemu ya pili kutoka Mitesa-Masasi (Km 60) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti kwa jumla ya Shilingi bilioni 92.548.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Masasi mjini Mhe. Geoffrey Mwambe amesema ujenzi wa barabara hiyo unakwenda kuwa mradi funganishi kuelekea mradi wa ujenzi wa standi kubwa ya kisasa ya mabasi ya Masasi.
“Tukae mkao wa kula uzinduzi wa mradi huu, ndio unapelekea rasmi kuanza mchakato wa mkandarasi wa ujenzi wa standi kubwa ya kisasa ya mabasi pale Masasi mjini, Masasi inakwenda kubadilika” amesema Mwambe
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo ilishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Wakuu wa wilaya, Wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri, waheshimiwa madiwani, wabunge wa majimbo yote kutoka Mtwara, Wakuu wa idara na vitengo kutoka halmashauri za Mtwara, wandarasi, wafanyakazi, watendaji wa Tanroads na wananchi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.