Vyama vya Siasa wilayani Masasi mkoani Mtwara vimetakiwa kuzingatia Sheria za Nchi zikiwemo sheria za Uchaguzi na sheria zote zinazosimamiwa na ofisi ya msajili wa Vyama vya Siasa ili kudumisha amani, utulivu na uzalendo katika kipindi hichi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Hayo yamebainishwa Oktoba 23, 2024 katika kikao cha elimu kwa umma kilichotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Afisa Usajili kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Ndg. Zabron Nswila amesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inajukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika maeneo yanayohusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sambamba na kuwa kiungo kati ya Serikali na vyama vya siasa.
Aidha amesema katika kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Msajili wa Vyama vya Kisiasa ni kiungo kati ya Serikali na vyama vya siasa.
Msimamizi Msaidizi Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Prosper Luambano amesema vyama vya siasa ni wadau muhimu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba ni muhimu vyama vya siasa kuzingatia wajibu wao ikiwemo kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi ili kudumisha ushiriki wa uchaguzi ambalo ni jukumu la msingi la chama cha siasa, kuboresha uhusiano mzuri baina ya wadau, utii wa sheria bila shuruti, uvumilivu wa kisiasa na kudumisha amani, utulivu na uzalendo.
Kikao hicho kilichofanyika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji Masasi kilihusisha Wenyeviti na Makatibu vyama vya siasa kutoka Wilaya ya Masasi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.