Mkurugenzi Halmashauri ya Mji wa Masasi, Bi. Erica Yegella amesema ushirikiano uliopo baina ya Halmashauri ya Enzkreis ya Nchini Ujerumani na Masasi Mji una manufaa makubwa katika utekelezaji wa maendeleo yaliyolengwa katika sekta ya afya, elimu, matumizi ya sola na utunzaji mazingira kwa wananchi.
Amesema ushirikiano huo unazidi kuimarika zaidi kutokana na uhusiano bora uliopo na utazidi kuimarika kimaendeleo kwa manufaa ya halmashauri ya Mji Masasi.
Amesema hayo Julai 24,2023 katika hafla fupi ya kuwakaribisha viongozi wa Halmashauri ya Enzkreis aliyoiandaa na kufanyika nyumbani kwa Mkurugenzi majira ya Jioni na kuhudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, Viongozi kutoka Enzkreis, Wafanyabiashara, na watumishi mbalimbali.
Aidha katika hafla hiyo, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu, afya, nishati, kilimo, uvuvi na miradi mbalimbali yenye malengo ya kudumisha maisha ya watanzania.
“ Ushirikiano uliopo baina yetu, unatokana na matunda bora yanayotengenezwa na Jemedari wetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa watanzania, lakini pia balozi wa Ujerumani hapa Nchini kwa kuendelea kuimarisha mahusiano bora ya kimataifa” Bi. Erica Yegella
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Halmashauri ya Enzkreis ya Nchini Ujerumani, Dkt. Hilde Neidhardt amesema mapokezi waliyoyapata katika awamu hii ni yakitofauti na yakipekee.
Amesema ushirikiano huo ulioanza miaka 12 iliyopita utazidi kuimarishwa kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo iliyopo na inayotarajiwa kuanzishwa baina ya halmashauri zenye ushirika.
Ujumbe kutoka Halmashauri ya Enzkreis nchini Ujerumani umeongozwa na Makamu wa Rais wa Enzkreis, Dkt. Hilde Neidhardt, mratibu wa ushirikiano huo, Bi. Angela Gewiese, Frank Stephan, Dkt. Jannis Hoek, Melissa Gewiese na Dkt. Till Neugebauer.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.