Makamu wa Rais Halmashauri ya Enzkreis ya Nchini Ujerumani, Dkt. Hilde Neidhardt amesema wamefurahishwa na mapokezi waliyoyapata Masasi mkoani Mtwara hususani kupelekwa kufanya utalii katika mto Ruvuma na Pori la Akiba Lukwika Lumesule linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.
Amesema hatua za halmashauri za Masasi Mji na Wilaya kuwapeleka kujionea utalii inazidi kuimarisha ushirikiano na mahusiano baina ya Enzkreis na Masasi.
Amebainisha hayo July 23, 2023 mara baada ya kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii katika pori la akiba Lukwika Lumesule ikiwemo wanyama, miamba ndani ya mto Ruvuma na pango la Habiba lenye historia ya kipekee.
Naye, Mratibu wa ushirikiano huo kutoka Enzkreis, Bi. Angela Gewiese amesema ushirikiano kati yaEnzkreis na Masasi ulianza miaka 12 iliyopita na umezidi kuimarika zaidi.
“mimi ndiye mratibu wa ushirikiano kati ya Enzkreis, mji wa Masasi, na halmashauri ya wilaya ya Masasi. Ushirikiano huu umekuwepo kwa miaka 12, na nimefurahishwa sana kutembelea eneo la hifadhi ya wanyama ya Lumesule kwa sababu wakati wa ziara yetu ya kwanza mwaka 2013, eneo hili lilikuwa halina kitu chochote. Kwa hivyo, tunavutiwa sana na maendeleo ya hifadhi hii ya wanyama na kushuhudia jinsi mambo yalivyobadilika kwa wakati huu, sasa tuna askari wa uhifadhi na jengo la maonyesho ambapo watu wanaweza kuja kutembelea. Ni jambo zuri sana kuona jinsi utalii unavyokua hapa”. Bi Angela.
Ujumbe kutoka Halmashauri ya Enzkreis nchini Ujerumani umeongozwa na Makamu wa Rais wa Enzkreis, Dkt. Hilde Neidhardt, mratibu wa ushirikiano huo, Bi. Angela Gewiese, Frank Stephan, Dkt. Jannis Hoek, Melissa Gewiese na Dkt. Till Neugebauer.
Ushirikiano baina ya Enzkreis na Masasi umezidi kuimarisha uboreshaji wa miundombinu ya umeme hususani matumizi ya nishati ya jua kwa kutumia sola yanayolenga kuboresha mazingira na miradi mbalimbali inayotekelezwa kutokana na ushirikiano huo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.