Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Erica Yegella amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuongeza tija katika utendaji kazi hususani katika ukusanyaji wa mapato.
Bi. Yegella amesema ukusanyaji wa mapato ndio chachu ya maendeleo na hivyo kuwataka watumishi wote kushirikiana kikamilifu ili kutimiza lengo hilo.
Amesema hayo July 10, 2023 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji masasi katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la utawala katika halmashauri hiyo.
“Kwenye upande wa mapato mweka hazina na timu yako na wakuu wa Idara na Vitengo nyinyi nyote mnahusika kwenye ukusanyaji wa mapato, shule zetu za private zinatakiwa zitoe mapato, hospitali zetu, maduka yetu, viwanda nk. vinatakiwa vitoe mapato vyote mviainishe vizuri” amesema
Mkurugenzi Yegella ameagiza kuwekwa kwa mageti ya chuma katika vipenyo vikuu vya barabara ili kuhakikisha lengo la ukusanyaji mapato linafanikiwa kwa ufanisi.
“..na sasa hivi afisa utumishi mjipange mnaweka mageti mangapi katika vipenyo vikuu, kwasababu ukusanyaji wa mapato ndio kiu yangu” amesema
Aidha ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuhakikisha yanazingatia taratibu, kanuni na sheria hususani katika kudumisha maadili ya kitanzania.
“kwa upande wa NGOs zote zinazofanya kazi katika shule zetu tuzijue , zisimamiwe na tujue wanafundisha nini kwa watoto wetu na tuzijue na ziwe zimesajiliwa, NGOs ambazo hazijasajiliwa hazitaruhusiwa katika halmashauri yetu” amesema
Kwa upande wao watumishi wameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mkurugenzi wa halmashauri ili kuhakikisha dhamira na malengo ya halmashauri yanatimia kwa ukamilifu.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.