Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala ameshangazwa na utendaji kazi wa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na Mkurugenzi wa Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu na watalaamu wake kwa kukamilisha miradi kwa wakati na ubora unaostahili huku akimuagiza Katibu Tawala Mkoa kuzileta Halmashauri zinazosuasua katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuja kujifunza Halmashauri ya Mji Masasi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema hayo leo 21 Juni, 2024 wakati wa ziara yake ya kuzungumza na watumishi sambamba na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Masasi hususani ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu nane ya vyoo katika shule ya sekondari Anna Abdallah.
“ Natambua uwepo wa Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Masasi, viongozi na watu wote, nashindwa niseme nini lakini jamani kuna watu wanatenda kazi, fedha imepokelewa tarehe 3/4/2024 leo jengo lipo hivi, nitoe shukurani na pongezi za dhati kwako Mhe,Mkuu wa Wilaya lakini Mkurugenzi na Timu yako yote ambayo inakusaidia katika uratibu, lakini wasimamizi kuanzia ngazi ya walimu, viongozi wa kata na wananchi wote kwa ujumla wake kwa kazi nzuri kama hii, RAS nikuombe katika wale ambao wanaosuasua katika miradi walete waje wajifunze Masasi, kazi ni nzuri”, Mhe Mkuu wa Mkoa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Ndg. Reuben Sixbert Jichabu amesema mbali na Ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu nane ya vyoo katika Shule ya Sekondari Anna Abdallah, siku hiyohiyo tarehe 3/4/2024 fedha ilipokelewa Masasi Day kwaajili ya Ujenzi wa madarasa matatu na matundu nane ya vyoo sambamba na Nangose, darasa moja na matundu nane ya vyoo ambapo shule hizo mbili ujenzi wake umekamilika kwa kila kitu kinachosubiriwa ni wanafunzi kuingia darasani kusoma.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Anna Abdallah, Mwl, Zamoyoni Adam amesema shule hiyo ilipokea fedha kutoka Serikali kuu tarehe 3/4/2024 zaidi ya shilingi milioni 110 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu nane ya vyoo.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 20/4/2024 na kwa mujibu wa mkataba unatakiwa kukamilika 20/7/2024 lakini kutokana na kasi ya utekelezaji wa mradi mradi huo unatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo 28/6/2024.
Aidha ametoa shukurani zake kwa Serikali katika kuhakikisha Mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni yanaboreshwa.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Jumuiya ya Shule ya Secondari Anna Abdallah inatoa shukurani zake za dhati kwa Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Shule ya Sekondari ili kutengeneza Mazingira mazuri ya ujifunzaji na ufundishaji mashuleni , Aidha jumuiya ya Shule ya sekondari inaendelea kutoa shukurani zake kwa Mhe. Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini na Mhe. Sospeter Nachunga, Diwani kata ya Napupa kwa ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa katika utekelezaji wa mradi”. Mwl.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.