Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe, Geoffrey Mwambe amefungua rasmi zahanati mpya ya kijiji cha Matawale Kata ya Matawale, Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara ikiwa ni ndani ya siku sita tu toka alipofungua zahanati mpya ya Machombe.
Hatua hiyo ameeleza kuwa ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wa Masasi Mji wanapata huduma bora za afya kwenye maeneo yao.
Ameeleza hayo, Novemba 24, 2023 wakati wa ufunguzi rasmi wa zahanati ya Matawale iliyopokea fedha kiasi cha Tsh milioni 150 kutoka Serikali kuu zilizotolewa kwa awamu tatu.
Mhe. Mwambe amewataka watumishi katika zahati hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kujitoa, ushirikiano, weledi na kuzingatia huduma bora sambamba na kuwaomba wananchi kuwapa ushirikiano watumishi hao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanajiunga na bima ya afya yenye gharama ya Tsh 30000 tu kwa mwaka kwa familia.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mhe. Hashim Namtumba amesema kuwa huo ni mwendelezo wa kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana na kuimarika na kwamba Halmashauri itakikisha inaendelea kuimarisha huduma za afya katika maeneo yote ya Mji Masasi.
Diwani wa kata ya Matawale, Mhe. Hamisi Mnela amesema ufunguzi wa kituo hicho ni alama kubwa kwa wananchi kwa kuwapunguzia umbali wa kutafuta huduma za afya huku akiwashukuru Wananchi, Rais Dkt Samia na Mbunge Mwambe kwa kuhakikisha zahanati hiyo inakamilika na kufunguliwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mji Masasi, Ndg. Andrea Kalinga amewapongeza wananchi wa kijiji cha Matawale kwa kujitoa kwa nguvu kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa kwakuwa mchango wao ni mkubwa ukiwa na thamani ya fedha kiasi cha zaidi ya Tsh milioni tatu.
Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Salum Gembe amesema zahanati hiyo ni ya kisasa na bora na tayari watoa huduma za afya wameshaanza kutoa huduma katika zahanati hiyo.
Katibu Mwenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya masasi Ndg. Twahili Mayola akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM wilaya, amesema wananchi wanashuhudia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye maeneo ya Mji Masasi ikiwa ni pamoja na miradi elimu, barabara, maji na afya.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.