Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauter John Kanoni amewataka watumishi wapya wa Halmashauri ya Mji Masasi kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na uzalendo ili kutimiza malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema uzalendo unakwenda sambamba na uvumilivu wa mazingira yoyote ya kazi hivyo wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kazi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mhe. Kanoni amesema hayo Agosti 4, 2023 katika kikao cha watumishi wapya wa halmashauri ya Mji Masasi kilichoandaliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Bi. Erica Yegella kwa lengo la kuzungumza na waajiriwa wapya wa halmashauri hiyo.
“Pigeni kazi, kikubwa ni kuvumilia katika hali yoyote hasa kipindi cha mwanzo wa ajira, muhimu zaidi ni kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira nyingi,” Dc Kanoni
Aidha amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imezidi kutoa ajira nyingi kwa watanzania hivyo ni muhimu waajiriwa kuwa mabalozi bora wa Rais katika utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Erica Yegella amesema kama kiongozi ataendelea kuhakikisha maslahi ya watumishi wote wa ngazi zote yanazingatiwa na kutekelezwa.
Amesema ni muhimu kwa kila mtumishi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali.
Katika kikao hicho, Bi. Yegella amepiga marufuku tabia ya watumishi wote kukaa sehemu ambazo sio rasmi (korido) badala yake mtumishi akifika kazini aende moja kwa moja kutekeleza majukumu ya kazi yake.
“Kuna tabia ya watumishi kufika ofisini asubuhi saa moja na nusu na kukaa kwenye korido huku wakiongea, nimepiga marufuku, ukifika ofisini nenda moja kwa moja ofisini kwako katekeleze majukumu yako, kama ni vikao vifanyike ndani ya ofisi sio kwenye korido”, Mkurugenzi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.