Mkuu wa Wilaya ya Masasi akiwakilishwa na Afisa Tarafa Halmashauri ya Mji Masasi, Ndg. Fikiri Lukanga ametambulisha rasmi mradi wa kituo cha Elimu ya Mazingira kwa wananchi uliogharimu zaidi ya Tsh milioni 242 huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Mazingira ya wawekezaji na wafadhili yanaboreshwa, Serikali ya Ujerumani Landratsamt Enzkreis, Wizara ya Maendeleo ya Ushirikiano wa Kiuchumi Ujerumani, Taasisi ya Engagement Global ya Ujerumani, Taasisi ya Service Agency Ujerumani pamoja na Taasisi ya TAREA kwa kuwezesha kituo hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mhe. Hamisi Nikwanya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri amesema ushirikishwaji wa wadau mbalimbali kama Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati, makundi maalumu, akina mama wajasiriamali na wananchi kwa ujumla katika utoaji wa elimu ya mazingira utaleta mabadiliko makubwa katika mazingira na mabadiliko hayo yaanzie katika maeneo ya karibu na kituo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mkuu wa Divisheni ya Utumishi na Utawala, Bi. Renalda Mbowe amesema mbali na Halmashauri ya Mji Masasi kuchangia viwanja viwili vyenye thamani ya Tsh milioni 20 katika Ujenzi wa hicho, Halmashauri itaendelea kuhakikisha ustawi wa kituo hicho unadumu na kuleta manufaa kwa jamii.
Diwani Kata ya Napupa, Mhe. Sospeter Nachunga amesema ujenzi wa kituo hicho utaleta mapinduzi katika kujenga uelewa na kuzuia uchafuzi wa Mazingira na utenganishaji wa taka katika jamii ya Masasi.
Kaimu Mkuu Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Bi. Anna Hokororo, amesema ujenzi wa Mradi wa Kituo cha Mazingira unaotekelezwa katika Mtaa wa Wapiwapi A kata ya Napupa unahusisha ujenzi wa ukumbi wa mafunzo, ofisi ya wataalamu wa Mazingira na Nishati, mgahawa, sehemu ya kupumzikia, jiko, vyoo, ujenzi wa uzio na kisima cha uvunaji wa maji ya mvua.
Amesema ili kulinda Mazingira, mradi huo umetumia chuma kwenye kupaua, milango na madirisha ili kupunguza matumizi ya mazao ya misitu ili kulinda Mazingira na kwamba Ujenzi wa kituo hicho umegharimu jumla ya Tsh milioni 242,763,254 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Enzkreis ya Ujerumani.
Meneja wa Kituo hicho, Bi. Catherine Tendeje amesema kituo hicho kimelenga kutoa elimu ya mazingira na kuimarisha ustawi wa viumbe hai na uoto wa asili kwa kujenga uelewa na uanzishwaji wa vitalu vya miti, nishati mbadala mfano biogas na solar, uelewa na utengenezaji wa matumizi ya majiko sanifu.
Mratibu wa Ushirikiano kutoka Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Kajuti Nyambi amesema ushirikiano huo ulianza mwaka 2011 ambapo Halmashauri ya Mji na Wilaya zimekuwa zikinufaika katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, elimu, mazingira, nishati mbadala (ufungaji wa Umeme wa Jua) na michezo kwa kupata misaada mbalimbali ya kimaendeleo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.