Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauteri John Kanoni leo Februari 10, 2025 amewapongeza watendaji wa kata 14 za Halmashauri ya Mji Masasi kwa kuhakikisha utekelezaji wa mkataba wa usimamizi wa afua za lishe unafikia malengo katika kipindi cha Robo ya pili, Oktoba hadi Desemba 2024/2025 kwa kupata “kadi alama” bora za utekelezaji.
Amesema pongezi hizo ziende sambamba na juhudi za kuhakikisha asilimia ya wanafunzi wanaopata walau mlo mmoja shuleni inaongezeka kwa kuhakikisha elimu zaidi inatolewa kwa wazazi na kutumia sheria kuhakikisha wazazi wanajitoa kwa dhati ili wanafunzi wapate mlo shuleni hali itakayosaidia kupata asilimia 100 za kadi alama na ufaulu wa wanafunzi shuleni.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Masasi, Dkt. Salum Gembe amesema mbali za jitihada hizo, kupitia Mkurugenzi wa Mji Masasi, utekelezaji wa mkataba umeongezeka zaidi baada ya kufikiwa kwa lengo la kutoa fedha za afua ya lishe zaidi ya Tsh milioni 12 kwa kipindi cha robo ya pili kati ya milioni 16 zilizotengwa kwenye bajeti ya mapato ya ndani.
Mratibu wa Lishe Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Happiness Mlamka amesema asilimia ya wanafunzi wanaopata walau mlo mmoja shuleni zimepanda kwenye Kata mbalimbali.
Amesema wataendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora na athari zitokanazo na lishe duni ili kuhakikisha malengo ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe yanafanikiwa.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.