Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano – Masasi Mji
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mheshimiwa Selemani Mzee amekabidhi mabati ishirini (20) yenye thamani ya shilingi 500,000/= kwa Serikali ya Kijiji na Kamati ya Shule ya Msingi Mbonde ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Gaspar Byakanwa aliyoitoa mnamo tarehe 30/01/2020 alipotembelea Shuleni hapo.
Makabidhiano hayo yamefanyikia Shule ya Msingi Mbonde iliyopo Kata ya Mwenge Mtapika, Halmashauri ya Mji Masasi. Wananchi wa Kijiji cha Mbonde waliibua mradi wa ujenzi wa matundu kumi (10) ya vyoo ikiwa ni sehemu ya kuitikia Kampeni ya Shule ni choo iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mwishoni mwa mwaka jana 2019.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mabati hayo, Mheshimiwa Mzee amewaasa Wananchi wa Mbonde kumtia moyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kumuonesha ya kwamba mchango wake huo ambao ameutoa kwenye Shule hiyo unatumika ipasavyo na kwa wakati ili kuwasitiri Wanafunzi wa Shule hiyo ya Msingi.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alitumia hadhara hiyo kuiagiza Halmashauri ya Mji Masasi ikamilishe miradi iliyoibuliwa kwenye Kampeni ya Shule ni choo ili Shule zitakapofunguliwa baada ya kuisha kwa janga la ugonjwa wa Covid-19, Wanafunzi wa Shule husika wakute miundo mbinu ya vyoo hivyo imekamilika.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ameagiza uongozi wa ngazi zote unaozisimamia Shule za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuhakikisha Shule zinafanyiwa usafi wa mazingira ili zitakapofunguliwa Wanafunzi waanze masomo, na siyo kutumia wiki nzima au zaidi kuyafanyia usafi mazingira ya Shule hizo. Aidha, amesisitiza kuimarishwa kwa ulinzi kwenye mazingira ya Shule zote ili kusitokee uharibifu wa mali na miundombinu ya Shule katika kipindi hiki cha likizo.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Mbonde, Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Mussa Zuberi Millanzi, alimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kuguswa na mradi huo wa matundu kumi (10) ya vyoo vya wanafunzi, na kwamba mabati hayo ishirini (20) yatatosha kuezekea jengo hilo la vyoo vya wanafunzi kulingana na bajeti. Aliahidi ya kwamba mabati hayo yaliyotolewa yatatumika kama ilivyokusudiwa.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.