Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano – Masasi Mji
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameipongeza Halmashauri ya Mji Masasi kutokana na kasi nzuri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Brigedia Jenerali Gaguti ametoa pongezi hizo leo tarehe 29/11/2021 baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi na kisha kutembelea Shule zinazotekeleza mradi huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ambazo ni Shule za Sekondari Nangaya, Chanikanguo, Mtandi, Mtapika, Marika, na kisha Kata ya Mtandi ambako kunajengwa Kituo cha Afya. Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa upo katika hatua za ukamilishaji wakati mradi wa Kituo cha Afya upo katika hatua ya kujenga boma.
Mhe. Mkuu wa Mkoa, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Ndugu Elias Ntiruhungwa kwa kusimamia vizuri ujenzi huo akisema kwamba Mkurugenzi huyo ni mfano wa kuigwa.
Halmashauri ya Mji Masasi ilipokea jumla ya shilingi milioni 820 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 37 vya madarasa pamoja na ujenzi wa Bweni moja la Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaosoma Shule ya Msingi Masasi.
Aidha, Halmashauri ya Mji Masasi ilipokea mgao wa fedha iliyotokana na tozo za miamala ya simu kiasi cha Shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kimkakati Kata ya Mtandi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mkuu wa Mkoa alipata wasaa wa kuongea na Wananchi wa Kata za Chanikanguo na Mwenge Mtapika ambapo amewasisitiza kulinda amani na usalama katika maeneo yao, kuwekeza katika Elimu ya watoto wao, na kushiriki kikamilifu katika miradi ya ujenzi inayoendeshwa kwenye maeneo yao kwa kujitolea.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa Mhe. Abdallah Mohamed Malela pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.