Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi Bi. Renalda Mbowe amesema hali ya utekelezaji wa afua za lishe kwa jamii inazidi kuimarika na kuboreshwa mara baada ya Halmashauri ya Mji Masasi kupanda kwa kasi kutoka nafasi ya nane kimkoa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hadi nafasi ya tatu kimkoa kwa mwaka 2023/2024 katika usimamizi wa utekelezaji wa afua za lishe.
Amesema hayo mara baada ya kukabidhiwa cheti cha pongezi kilichotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala na kukabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mji na Mratibu wa Lishe Masasi Mji Bi. Happiness Mlamka ambapo Halmashauri ya Mji Masasi imepata cheti cha pongezi kwa kuibuka mshindi wa tatu katika usimamizi wa utekelezaji wa afua za lishe kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Aidha amewataka watalaam kuendelea kuimarisha usimamizi wa afua za lishe kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora na athari zitokanazo na lishe duni ikiwemo udumavu, magonjwa yasiyoambukiza na kuhamasisha jamii kuhusu upatikanaji wa chakula shuleni ili Halmashauri iendelee kupanda kwa kasi kimkoa na kitaifa kwa ujumla.
Hayo yamejiri leo Februari 25, 2025 katika kikao cha Kamati ya Lishe Robo ya Pili, 2024/2025 kilichofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Utawala ambapo watalaamu wameeleza taarifa za lishe kwa upande wa elimu ya awali na msingi, elimu sekondari, kilimo, mifugo na uvuvi, Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.
Kikao hicho kimejadili kwa kina hali ya lishe shule za msingi na sekondari, hali ya utapiamlo, matibabu ya utapiamlo mkali, unyonyeshaji maziwa ya mama ndani ya lisaa la kwanza, Watoto waliozaliwa na uzito pungufu, Watoto wanaopata chakula shuleni na ukaguzi na uhamasishaji wa matumizi ya vyakula vilivyoongezewa virutubishi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.