Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Machi 21, 2024 imeendelea na zoezi la kuwanoa maafisa ugani wa sekta ya Mifugo waliopo kanda ya kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye mafunzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Utawala, Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauter Kanoni amewasisitiza maafisa ugani hao kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo kwenda kubadili mfumo wa ufugaji kutoka ule wa holela hadi ufugaji wa kisasa.
"Wakati wa msimu wa mvua hali ni shwari lakini ikifika kiangazi sisi na nyie Maafisa Mifugo huwa hatulali kila kukicha tunaenda kushughulikia migogoro baina ya wakulima na wafugaji hivyo tumieni mafunzo haya kuwabadili wafugaji waanze kufuga kisasa ili kuepusha madhara baina ya pande hizo mbili" Amesisitiza Mhe. Kanoni.
Aidha Mhe. Kanoni amewataka watalaam hao katika sekta ya Mifugo kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo kwa mifugo ili kuepusha madhara kwa mifugo na watumiaji wa mazao ya Mifugo hiyo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzake, Daktari wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bi. Subira Simbeye ameahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Kanoni ili kuendelea kuboresha sekta ya Mifugo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Awali akiwasilisha mada ya "Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma", Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizarani hapo Bi. Suzan Silayo amewataka Maafisa ugani hao Kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia maadili ya utumishi na kufuata sheria kanuni na taratibu za kiutumishi.
"Pia mkafanye kazi bila upendeleo na muwe waaminifu wakati wote huku mkitoa ushauri kwa viongozi wenu pale inapobidi kwa kuwa wao nyie ndio wataalamu lakini wakati wote msisahau kutunza siri za serikali" Ameongeza Bi. Silayo
Aidha Bi. Silayo amewataka wataalam hao kuepuka kutoa au kupokea rushwa huku pia akiwasisitiza kujiandaa na maisha ya baada ya kustaafu katika Utumishi wa Umma kwa kuhakikisha wanafanya uwezekaji wa kutosha pindi wakiwa kazini.
Mafunzo hayo kwa Maafisa Ugani wa mikoa ya kanda ya Kusini yatafanyika kwa siku 2 ambapo mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa kwa wataalam hao kwa lengo la kuwakumbuka taratibu mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yao pindi wakiwa uwandani.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.