Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Erica Yegella amesema kipaumbele cha kwanza atakachokisimamia katika mwaka wa fedha 2023/2024 ni ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani uweze kutekelezeka na kukamilika kwa wakati.
Amesema hayo Agosti 3, 2023 ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria na kushiriki mkutano wa Baraza la Madiwani Robo ya nne 2022/2023 uliofanyika katika ukumbi wa Jengo la Utawala.
Amewaomba waheshimiwa madiwani kutoa ushirikiano katika maeneo yao hususani katika ukusanyaji wa mapato kwa kuwa wao ni wenyeji wa vipenyo vya mapato.
“Na niwe wazi kwenu waheshimiwa madiwani mimi natafuta mapato ili nikatekeleze miradi hususani miradi ya mapato ya ndani, na ukweli usiopingika sitadandia mradi, nitatekeleza yale mliyoagiza kwenye bajeti” Mkurugenzi.
Katika Baraza hilo, Bi. Yegella amesema ataendelea kusimamia kwa ukamilifu utendaji kazi wa watumishi ili kila mmoja awajibike kwa ukamilifu na weledi.
“Niwashukuru sana sijawahi kuona Baraza zuri la Madiwani kama hili, baraza pendwa na linasema ukweli, na mimi kama mtendaji inanipasa nikawajibike, nimeyasikia yote na nimeyapokea,”
Amesema hatasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote atakayekwenda kinyume na taratibu, sheria, kanuni na miongozo ya utendaji kazi ili Halmashauri itekeleze miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
“Mimi mheshimiwa Mwenyekiti sitakuwa na maneno mengi, ninatabasamu sana ila kumunyoosha mtu sioni shida, mimi ninafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo” Bi Erica.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.