Kamati ya Lishe Halmashauri ya Mji Masasi imepongezwa kwa kuwezesha utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa chakula shuleni kwa asilimia 100 huku ikitakiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wazazi na jamii juu ya umuhimu wa wazazi kuchangia upatikanaji wa chakula ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa lishe bora shuleni.
Pongezi hizo zimetolewa Julai 26, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Ndg, Andrea Kalinga akimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya lishe (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji), wakati wa kikao cha kamati ya Lishe Robo ya Nne 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Jengo la Utawala Masasi Mji.
Amesema pamoja na hilo elimu kupitia vikao na wazazi, walezi na jamii inatakiwa kuendelea kutiliwa mkazo ili wazazi wote watambue kwa kina umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi wote sambamba na kuendeleza bustani za mbogamboga, miti ya matunda na kupanda mimea jamii ya kunde katika maeneo ya shule ili kuchangia upatikanaji wa lishe bora shuleni.
“lakini pia tukaangalie namna ya kufanya hasa kuongea na wadau kama Sanku kwakuwa anatoa mashine za kuchanganya virutubisho kwenye unga wa kusaga, virutubisho, na mifuko ya kufungasha, basi tuombe hata mashine ili waweze kuongeza virutubisho hivyo kwa ajili ya vyakula vya wanafunzi ” Ndg. Kalinga
Awali, akieleza kuhusu utekelezaji wa afua za lishe kwa shule za msingi na sekondari, Mratibu wa Lishe Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Happiness Mlamka amesema jumla ya shule zinazotekeleza mpango wa upatikanaji wa chakula shuleni ni 56 ambazo ni sawa na asilimia 100 kwa kuwa ndio jumla ya shule za msingi na sekondari zinazopatikana katika halmashauri hiyo.
Amesema suala la lishe ni suala mtambuka hivyo ni muhimu ushiriki wa kila mmoja katika taasisi na jamii kujitoa kwa dhati ili kutimiza malengo ya upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi wote kwani asilimia 41.66 ndio waliopata chakula kwa mwaka 2022/2023.
“Suala la lishe jamani ni suala mtambuka, wote hapa tunapaswa kujitoa kwa dhati kwa kuweka shughuli za kufanya (activity) katika idara zetu, kuanzia maendeleo ya Jamii, Elimu, Kilimo na uvuvi lakini kama fedha imetengwa kwa ajili ya lengo (objective Y) itumike kukamilisha lengo Y pekee na sio kuhamisha hamisha fungu, tuzidi kuzingatia hili ili tuzidi kupata alama” Bi. Happiness
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.