Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hashim Namtumba amezindua rasmi jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi na kukabidhi mwongozo wa uendeshaji wa jukwaa hilo kwa ngazi ya Halmashauri.
Amezindua na kukabidhi mwongozo wa uendeshwaji wa jukwaa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ngazi ya Halmashauri Bi. Mariam Ngole, Novemba 9, 2023 katika ukumbi wa Jengo la Utawala.
Mhe. Namtumba, amesema malengo ya uanzishwaji wa jukwaa hilo ni utekelezaji wa malengo 17 ya dunia kati yake ni yale yanayohimiza ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za maendeleo na za kijamii na ushirikishwaji wa 50/50.
Amesema malengo hayo yanasimamiwa vyema na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan na kwamba jukwaa hilo litakuwa endelevu na litapata uungwaji mkono kutoka halmashauri.
"Jukwaa hili tunaamini litakuwa endelevu na litasimama vizuri sana, sisi kama halmashauri hatutatenda haki kama tutawaacha muende pekee yenu, ni lazima sisi tushiriki kwa nafasi yetu kama halmashauri, leo tumezindua na kutoa mwongozo wa uendeshaji wa jukwaa hili" Mhe. Namtumba.
Amesema lengo ni kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa katika ngazi za uongozi, utawala na uchumi.
Katibu wa Umoja wa wanawake wilaya ya Masasi, Martina Katyale amesema pamoja na mambo mengine lengo la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wanawake ambao wapo hali ya chini na kuwainua kiuchumi ili waweze kulingana na wanawake wote kiuchumi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi Halmashauri ya Mji Masasi, Mariam Ngole amesema wanawake wasisite kumfikia kwaajili ya utekelezaji, ukuaji na ustawi wa jukwaa hilo na kwamba atashirikiana na kila mwanamke kwa kutoa elimu, maoni na mawazo ili wanawake wote wakuze uchumi wao.
Jukwaa hilo katika ngazi ya halmashauri linaongozwa na Mwenyekiti wake, Mariam Ngole, Makamu mwenyekiti Mwajuma Kamundi, katibu wake Bi. Leah Amuli, Katibu msaidizi Agnes Zawadi na Mweka hazina, Mwajuma Dadi na wajumbe.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.