Jumla ya Tsh Milioni 148 zimetolewa kwa vikundi 30 katika Hafla ya Utoaji wa Mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu iliyotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani Halmashauri ya Mji Masasi kwa awamu ya pili mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia na kurejesha mikopo hiyo ili kuwasaidia wananchi kiuchumi.
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi, April 7, 2025 katika utoaji wa mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu amesema zaidi ya Tsh milioni 545 zimetolewa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa vikundi 105 ambapo awamu ya kwanza vilipokea vikundi 75 na hivi sasa vikundi 30.
Amesema mafanikio hayo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamefikiwa na kuandika historia hiyo kutokana na usimamizi mzuri kutoka kwa viongozi mbalimbali, Baraza la Madiwani chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Hashim Namtumba na Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe. Geoffrey Mwambe hususani kuhakikisha wananchi wanaimarika kiuchumi.
Akikabidhi hundi ya Tsh milioni 148 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Rachel Kassanda amesema kuwa lengo la kutoa fedha hizo hadharani ni kuwafanya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu waone umuhimu wa kuanzisha vikundi ili wapate fursa za kupata mikopo hiyo ili wastawi kiuchumi na kijamii.
“Imani yangu kubwa tutakapo kusanya fedha zingine tena tutaleta hundi kwa ajili ya vijana wengine wapya,wanawake pamoja na watu wenye ulemavu, ni muhimu tufanye kazi kwa kuwa Serikali imeendelea kutengeneza mazingira bora ya kiuchumi kwa wananchi” amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hashim Namtumba amesema waheshimiwa madiwani wamefanya kazi muhimu kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa ili kuwezesha ustawi wa wananchi na kwamba hakuna kikundi kilichopata kwa upendeleo na hivyo vikundi vyote vikawe mabalozi wa kusema mazuri ya Serikali na Halmashauri.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Bi. Neema Joseph amesema katika vikundi 30, wanawake wamepokea Tsh 77,800,000 kwa vikundi 17, Vijana Tsh 68,000,000 kwa vikundi 11 na watu wenye ulemavu Tsh milioni 2,200,000 kwa vikundi viwili.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.