Zaidi ya Watumishi 200 kutoka Halmashauri ya Mji Masasi na Nanyamba leo Jumamosi wameshiriki kwenye Bonanza la Michezo lililofanyika kwenye Uwanja wa Boma Masasi Mjini. Bonanza hilo lilikuwa na lengo la kudumisha mahusisano mema kazini, Kujenga ushirikiano na mshikamano, na kuwaweka Watumishi wa Umma katika afya njema ili kuepuka magonjwa nyemelezi.
Bonanza hilo lilihusisha michezo ya Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete (Netball), Mpira wa wavu (Volleyball), Kuvuta kamba, Kufukuza kuku, na Kukimbia kwa kutumia gunia.
Katika bonanza hilo ambalo lilionekana kuwa na upinzani mkubwa kutokana na umahiri mkubwa uliooneshwa na wachezaji wa michezo mbalimbali kutoka kwenye Halmashauri zote mbili, matokeo ya mpira wa miguu Halmashauri ya Mji Masasi waliibuka kidedea baada ya kushinda goli mbili bila, Mpira wa Pete (Netball) Halmashauri ya Mji Masasi pia waliibuka washindi baada ya kuwafunga Halmashauri ya Mji Nanyamba kwa magoli 25 kwa 5, Kwenye mpira wa wavu (Volleyball) nako Halmashauri ya Mji Masasi waliibuka na ushindi wa seti mbili bila dhidi ya Halmashauri ya Mji Nanyamba, mchezo wa kuvuta kamba ambao uliwashindanisha wanawake peke yao Halmashauri ya Mji Masasi walibeba ushindi; Wakati Halmashauri ya Mji Nanyamba wakiibuka washindi kwenye kufukuza kuku na kukimbia ndani ya gunia (Wanaume), Halmashauri ya Mji Masasi wanawake waliibuka kidedea kwenye kukimbia ndani ya gunia.
Akifungua Bonanza hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji Masasi, Ndugu Richard Boniface Didas ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Masasi aliwashukuru Watumishi wa Halmashauri zote mbili hususani Halmashauri ya Mji Masasi ambao walikuwa wenyeji kwa kujitokeza kwa wingi na kuwahimiza kufanya mazoezi mara kwa mara kwa ajili ya kujenga, kulinda na kuimarisha afya zao. Alikazia ya kwamba mazoezi kwa Watumishi wa Umma na Wananchi kwa ujumla kila Jumamosi ya pili ya kila mwezi ni agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan linalotakiwa kutekelezwa kwa vitendo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.