Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Masasi limejadili na kuidhinisha rasimu ya mapendezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Halmashauri hiyo inakadiria kupokea na kutumia jumla ya Tsh. 30,195,139,106.07.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani la kujadili na kupitisha bajeti hiyo Februari 29, 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hashim Namtumba amesema bajeti hiyo imezingatia mapendezo yote muhimu ya waheshimiwa madiwani na hivyo itakwenda kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe, Geoffrey Mwambe amesema bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vya wananchi wa Masasi Mji.
Amesema mbali na bajeti hiyo bado anaendelea kupambana kwa dhati kuhakikisha ujenzi wa masasi mpya unawafikia wananchi wa Masasi Mji katika kata zote 14 kupitia uboreshaji wa miundombinu ambapo barabara ya kisasa yenye miradi funganishi kama stendi ya kisasa inakwenda kujengwa sambamba na maboresho ya kisasa katika standi ya uwanja wa fisi (ambayo ameshauri maboresho yakishafanywa jina libadilishwe), sambamba na ujenzi na maboresho katika eneo la Sokosela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu amesema katika jitihada za kuongeza mapato ya ndani, katika mwaka wa fedha 2024/2025 wanatarajia kujenga hoteli ya kisasa yenye kumbi kubwa tatu za mikutano na kumbi ya starehe sambamba na kuboresha miundombinu ya shule, kuwezesha wananchi kiuchumi,kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji, Mkuu wa divisheni ya Mipango na Uratibu Halmashauri ya Mji Masasi, Ndg. Prosper Luambano amesema Halmashauri inakadiria kupokea na kutumia jumla ya shilingi 30,195,139,106.07 kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Amesema vyanzo hivyo ni mapato ya ndani shilingi 3,397,212,700.00, matumizi mengineyo shilingi 1,040,957,000.00, Mishahara-shilingi 18,764,926,000.00, Miradi ya maendeleo (Serikali kuu na Wahisani) shilingi 6,992,043,406.07
Amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni kuongeza mapato ya ndani kutoka Tshs 2.8 Billion ya sasa hadi Tshs Billioni 3.4., Kuimarisha shughuli za utawala bora, Kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, Uimarishaji wa usafi wa mazingira, Kuboresha miundombinu ya shule za Msingi, Uwezeshaji wananchi kiuchumi, Ukamilishaji wa miradi viporo, Umilikishaji wa maeneo ya umma.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa Mkutano wa kujadili na kuidhinisha rasimu ya mpango wa bajeti Halmashauri ya Mji Masasi kwa mwaka wa fedha 2024/2025
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.