Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Masasi limejadili na kuidhinisha rasimu ya mapendezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo Halmashauri hiyo inakadiria kupokea na kutumia jumla ya Tsh. 25,987,919,626.27.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani la kujadili na kupitisha bajeti hiyo Februari 12, 2025, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hashim Namtumba amesema bajeti hiyo imezingatia mapendezo yote muhimu ya waheshimiwa madiwani na hivyo itakwenda kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu amesema katika jitihada za kuongeza mapato ya ndani, katika mwaka wa fedha 2025/2026 wametenga bajeti ya ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao, kuboresha mazingira kwa kununua gari la majitaka, ununuzi wa kifaa cha upimaji wa ardhi (RTK) sambamba na kuboresha miundombinu ya shule, kuwezesha wananchi kiuchumi,kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji, Kaimu Mkuu wa divisheni ya Mipango na Uratibu Halmashauri ya Mji Masasi, Ndg. Petro Marwa amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026 Halmashauri ya Mji Masasi inatarajia kukusanya, kupokea na kutumia jumla ya shilingi 25,987,919,646.27 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato.
Amesema Kati ya kiasi hicho Shilingi 5,582,087,256.07 ni ruzuku ya maendeleo ambapo kiasi cha Shilingi 1,996,867,952.56 ni ruzuku ya maendeleo kwa vyanzo vya ndani (Development Local) na Shilingi 3,959,289,256.07 ni ruzuku ya maendeleo kwa vyanzo vya nje (Development Foreign). Kiasi cha shilingi 15,452,240,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi 1,454,463,000.00 ni matumizi mengineyo.
Amesema vyanzo hivyo ni mapato ya ndani shilingi 3,499,129,390, matumizi mengineyo shilingi 1,040,957,000, Mishahara-shilingi 15,452,240,000, Miradi ya maendeleo (Serikali kuu na Wahisani) shilingi 5,582,087,256.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.