Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Reuben Sixbert Jichabu leo Septemba 01, 2025 amekutana na kuzungumza na mafundi ujenzi wote wa Halmashauri ya Mji Masasi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo vibali vya ujenzi na hamasa ya mafundi hao kujiunga na mfumo wa Manunuzi (NeST) ili kuweza kupata tenda mbalimbali za Serikali.
Akizungumza na mafundi waliojitokeza kwa wingi katika ukumbi mkubwa wa Jengo la Utawala amesema ni muhimu mafundi ujenzi kuwakumbusha wamiliki wa nyumba wanazojenga kukata “KIBALI CHA UJENZI” Halmashauri ya Mji Masasi kwa kuwa ni takwa la kisheria.
“Tumewaita mafundi na kuwapa elimu hii ili mnapopewa kazi za ujenzi, kabla ya kuanza kujenga muwakumbushe wamiliki wa hizo nyumba kwa kuwaomba kibali cha ujenzi, na muhimu copy ya kibali iwe site, hii ni kwasababu wananchi wengi wanajenga pasipo kuwa na kibali cha ujenzi, kwamfano tumepita kata mbalimbali ukienda kata ya Mkuti, tumetembelea nyumba zinazojengwa zaidi ya 200 lakini zenye vibali ni nyumba zaidi ya 10 tu..kwahiyo ni muhimu sisi kwenda kuwahimiza wamiliki kukata kibali cha ujenzi Halmashauri ya Mji Masasi” amesisitiza.
Wakizungumza watalaamu mbalimbali katika kikao hicho wamesema kibali cha ujenzi kinapatikana kwa haraka bila changamoto zozote kwa kuwa kwa mujibu wa sheria kibali kinapatikana kuanzia siku 0-7 toka unapoomba kibali.
Kwa upande wao Mafundi ujenzi mbalimbali wamempongeza Mkurugenzi wa Mji kwa kuwaita na kuwapa elimu muhimu ya vibali vya ujenzi na mfumo wa NeST na kwamba watakwenda kuwahimiza wamiliki wa nyumba wanazojenga kuhakikisha wanakata kibali cha ujenzi ili waweze kuendelea na ujenzi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.