Halmashauri ya Mji Masasi kupitia Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe imeanzisha utaratibu wa kuwatambua watumishi wa afya na vituo vya kutolea huduma za afya kwa kutoa zawadi na vyeti vya pongezi ikiwa ni mpango mkakati wa kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kutokomeza vifo vya mama na watoto wachanga.
Zawadi hizo zimetolewa April 9, 2024 katika kikao cha tathmini ya Januari- Machi 2024 cha afya ya uzazi wa mama na mtoto kilichofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Utawala Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Kaimu Mkurugenzi wa Mji Masasi Ndg. Andrea Kalinga amesema mpango huo ni bora na muhimu katika kutokomeza vifo vya mama na mtoto huku akisisitiza kuhakikisha mikakati mbalimbali inasimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Masasi, Dkt. Salum Gembe amesema utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza umeanzishwa rasmi kupitia mawazo bora ya timu ya usimamizi wa huduma za afya (CHMT) ili kuongeza ufanisi wa utoaj huduma, ili kutokomeza vifo vya mama na watoto.
" Watumishi hawa wanajitoa sana, wanafanya kazi masaa 24, wakati mwingine wanaingia kwenye shida za kitaaluma au kiutumishi, kwasababu wamebeba jukumu la kuokoa afya za watu.Tumeanzisha utaratibu wa kuwatambua kwa kuwapongeza kwa barua na vyeti, wote wanafanya kazi vizuri lakini leo tutapata ambao watatuwakilisha na hili zoezi litakuwa endelevu "amesema.
Katika zawadi hizo, kituo cha afya Mbonde kimepata cheti kwa kutopata kifo cha mama na watoto wachanga kwa kipindi cha Januari- Machi 2024 na watalamu wa afya waliopata barua za pongezi, Dr. Hashimu chiwaya( Mkomaindo Hospital) Hassani chande(Zahanati ya mumbaka) Atika mussa (Mkomaindo hospitali) na Edina mkwango (Mkomaindo hospitali)
Aidha, Dkt. Gembe amesema mbali na jitihada hizo mikakati mbalimbali imewekwa ikiwa ni kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za akina mama wote wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma, kuimarisha mfumo wa usafirishaji, kukusanya damu salama, na kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya ili kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma.
Matukio mbalimbali katika picha.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.