Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Masasi leo tarehe 6/12/2018. Akiwa ziarani Masasi, Waziri Ummy amehutubia wakazi wa Masasi katika eneo la Mti Mwiba mjini Masasi. Katika hotuba yake kwa wakazi wa masasi Mhe. Ummy ameongelea upatikani wa dawa muhimu katika Hospitali ya Mkomaindo kuwa kwa sasa ni zaidi ya asilimia 90.
Katika uimarishaji wa huduma za Afya Waziri Ummy amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Masasi Mhe.Rashid Chuwachuwa ili kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Masasi katika masuala ya afya.Katika kutatua kero mbalimbali zinazoikabili Hospitali ya Mkomaindo ikiwemo uchakavu wa gari la kubebea wagonjwa, Waziri Ummy amehaidi kutoa gari moja la kubebea wagonjwa kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Mkomaindo.
Sambamba na uimarishaji wa huduma za afya Waziri Ummy amewataka wananchi wa Masasi kujiunga na Bima ya Afya ijulikanayo kama Ushirika Afya mahususi kwa ajili ya wakulima pindi wanapopata fedha zinazotokana na malipo ya korosho. ”Tuweke utaratibu wa kuwa na uhakika wa matibabu “alisema Waziri Ummy. Bima hii inasimamiwa na Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka wananchi wa Masasi kuzingatia kanuni za afya kwa kujenga vyoo bora ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, “kinga ni bora kuliko tiba” alisema Waziri Ummy na kuitaka kila kaya kuwa na choo bora.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.