Walimu wa awali Halmashauri ya Mji Masasi wamepewa mafunzo juu ya Matumizi ya njia na utengenezaji wa zana za kufundishia zitakazosaidia kwenye utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Awali ulioboresha kupitia Mradi wa Boost.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Januari 9, 2025 hadi Januari 12, 2025 katika Shule ya Msingi Mkomaindo yakilenga kwenye matumizi ya njia na vifaa vilivyoboreshwa vya mtaala wa elimu ya awali.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Hamida Msemo amewataka walimu wa awali kutumia zana hizo ipasavyo ili ziweze kuleta tija na matokeo yanayoridhisha huku akiwasisitiza kuhakikisha wanafunzi wote wanaoingia darasa la kwanza waweze kusoma, kuandika na kuhesabu kama ambavyo mwongozo unataka.
Naye, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo na Mkufunzi kutoka Chuo Cha Ualimu Vikindu Bi.Naomi Mjema amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza umahiri katika kutekeleza Mtaala ulioboreshwa na muhtasari wa elimu ya awali pamoja na kupitia miongozo mbalimbali ya Elimu ya awali.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Boost Halmashauri ya Mji Masasi Bi. Felister Chikomele amesema kuwa lengo la mradi huo wa boost ni kujenga msingi mzuri wa watoto kuanzia chini ambapo watoto watanufaika kupitia walimu waliopata mafunzo hayo ambao watasaidia wanafunzi kuingia darasa la kwanza wakiwa na uwezo wa kuandika, kusoma na kuhesabu.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.