Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara CPA. Bahati Geuzye ameziagiza Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinaweka kipaumbele katika utoaji wa huduma za Tiba Okovu na Huduma Msingi kwa Wagonjwa Mahututi (Essential Emergency and Critical Care) ambayo ni huduma nafuu na yenye ufanisi.
Amesema hayo Mei 15, 2025 wakati akifungua mafunzo ya watoa huduma za afya wapatao 144 yanayofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) yanayohusu Tiba Okovu na Huduma Msingi kwa Wagonjwa Mahututi (Essential Emergency and Critical Care) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mwambe Royal Court Halmashauri ya Mji Masasi.
Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuboresha huduma za afya kwa kutoa fedha nyingi katika Mkoa, Wilaya na Halmashauri za Mtwara hususani ujenzi wa miradi ya afya, ununuzi wa vifaa tiba, kuwezesha upatikanaji wa dawa kwa wingi na ajira mpya kwa watoa huduma za afya.
Akizungumza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Peter Majura Esanju amesema mafunzo hayo yanalenga kuokoa Maisha ya wagonjwa mahututi katika ngazi zote za kutolea huduma za afya hususani ngazi za msingi ambazo ni zahanati, kituo cha afya na hospitali za Halmashauri yakihusisha watumishi 144 wanaopata mafunzo kwa awamu kutoka Manisipaa ya Mtwara Mikindani na Nanyumbu kwa kuanzia na hadi sasa waliopata mafunzo ni watumishi 82.
Naye, Mshauri wa Ufundi kutoka UNICEF, Frank Eetaama amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika mambo mengi katika sekta ya afya ikiwemo huduma za mama na mtoto, uimarishaji wa mifumo na mafunzo mbalimbali yakiwemo ya Tiba Okovu na Huduma Msingi kwa Wagonjwa Mahututi (Essential Emergency and Critical Care) na kuomba ushirikiano huo kuendelea ili kunufaisha wananchi kwa huduma mbalimbali.
Picha mbalimbali za Matukio katika mafunzo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.