Viongozi mbalimbali wa Serikali wameipongeza Halmashauri ya Mji Masasi kwa kupata hati safi (Unqualified Opinion) katika taarifa ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumza June 13, 2023 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la kupitia taarifa za Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed aliwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa ya usimamizi wa miradi mbalimbali ya serikali.
Alisema usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye ngazi ya halmashauri na kata ni jukumu la kila mmoja bila kuwaachia watu wachache.
“Lakini niwapongeze zaidi kwa kupata hati safi (Unqualified Opinion)… lakini pia Halmashauri ihakikishe miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yake inakamilika kwa wakati uliopangwa ili kuondokana na hoja zinazotokana na halmashauri kushindwa kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa,” Mkuu wa Mkoa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Lauter John Kanoni alisema hati safi ndio kipimo cha utendaji na kuwapongeza waheshimiwa madiwani kwa kusimamia utendaji wa halmashauri hiyo uliosababisha kupatikana kwa hati safi huku akiwataka watendaji kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
“Nawapongeza Halmashauri ya Mji Masasi kwa kupata hati safi, na ndio kipimo, tungekuwa na hati isiyoridhisha hapa kila mtu uso wake usingekuwa na tabasamu, hii inadhihirisha kuwa waheshimiwa madiwani mnasimamia halmashauri vizuri” Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Masasi, Mhe. Mariam Kasembe aliwataka watendaji na menejimenti kuongeza juhudi ili mwaka ujao wa fedha halmashauri ipate hati safi nyingine.
“La mwisho, naomba nipongeze kwa kupata hati safi, naomba tukaze buti mwaka kesho msituangushe tupate hati safi tena,” Mwenyekiti wilaya CCM.
Akitoa taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Erica Yegella alisema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja sita huku hoja moja ikiwa imefungwa na tano zikiendelea.
“Halmashauri ya Mji imepokea taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali inayohusu mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2022, taarifa hii imelenga kuwajulisha matokeo ya ukaguzi na mapendekezo yaliyotolewa wakati wa ukaguzi, katika taarifa hiyo halmashauri ya Mji imepata hati safi,” Bi. Erica Yegella.
Awali, Kaimu Mkaguzi mkuu wa nje, Mkoa wa Mtwara, Bi. Mary Wembe alisema katika kipindi chote cha ukaguzi ofisi ya mkaguzi ilipata ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi na menejimenti ya halmashauri ya mji Masasi.
“kwa niaba ya ofisi ya taifa ya ukaguzi ya hesabu za serikali napenda kuwapongeza halmashauri ya Mji Masasi kwa kupata hati safi,”-Mary Wembe.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano jengo la utawala, Halmashauri ya Mji Masasi.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.