Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hamisi Nikwanya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri leo Januari 8, 2025 amezindua rasmi zoezi la kampeni ya uhamasishaji wa chanjo ya Mifugo itakayotolewa kwa ruzuku na Serikali dhidi ya magonjwa matatu ya mifugo kwa Ng`ombe (Homa ya mapafu), Mbuzi, Kondoo (Sotoka) na Kuku (Kideri) ambapo uhamasishaji wa chanjo hiyo utafanyika kwenye kata 14, vijiji 31 na Mitaa 57 ya Halmashauri ya Mji Masasi.
Amesema uhamasishaji huo ni jitihada na juhudi kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa chanjo za mifugo kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 jumla ya Tsh Bilioni 28.1 zimetolewa ili kufanikisha zoezi hilo.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi Ndg. Andrea Kalinga amewataka watalaam waliojengewa uwezo kuhusu zoezi la utoaji wa chanjo ambao ni maafisa mifugo, uvuvi na kilimo Kwenda kufanya kazi kwa kujitoa kwa dhati na uadilifu wa kiwango cha juu ili kuweza kuwasaidia wafugaji.
Akieleza kuhusu mpango huo Daktari wa Mifugo Halmashauri ya Mji Masasi Dkt. Vailet Mhehe amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa mpango wa miaka mitano wa kutoa chanjo dhidi ya magonjwa matatu ya mifugo kwa wakati mmoja Nchi nzima kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo ambayo ni Homa ya Mapafu ya Ng`ombe (CBPP), Sotoka kwa mbuzi na kondoo (PPR) na Kideri kwa Kuku.
Amesema katika mpango huo, wafugaji watachangia gharama ndogo sana ya utoaji wa chanjo hizo ambapo Ng`ombe ni Tsh 500, Mbuzi na Kondoo Tsh 300 na kwa Kuku chanjo itatolewa bure, kuanzia Januari 25, 2025.
Ameongeza kuwa faida za utoaji wa chanjo hiyo ni pamoja na kupunguza vifo vya mifugo, kuwapunguzia wafugaji gharama za kununua chanjo wenyewe, kuongeza soko la mifugo ndani na njee ya Nchi, kutoa ajira za moja kwa moja na kuwezesha viwanda vinavyotumia mifugo au mazao ya mifugo.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.