Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa ngazi zote kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuacha tabia ya kukaa maofisini.
Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo Septemba 17, 2023 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Boma uliopo Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara .
Ameeleza kusikitishwa kuona kero za Wananchi wa Vijijini zinafika mpaka Ikulu wakati kwenye maeneo yao kuna Viongozi wa ngazi zote.
Mhe. Rais amesema,
“Nitoe wito kwa Uongozi mzima wa Mkoa na ngazi zote hadi Uongozi wa Vijiji na Mtaa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi, Waziri wa TAMISEMI amelisema vizuri hapa nami naomba nimuunge mkono, mtakaposhuka jamani, nyinyi sio Watawala, hata Mimi sio Mtawala, Mimi ni Mtumishi wa Wananchi, Mawaziri wangu ni Watumishi wa Wananchi, tuliowashusha chini huku kutuwakilisha ni Watumishi wa Wananchi”
“Unapoacha kiti cha Utumishi ukakaa kiti cha Utawala ndio maana huwezi kushuka kwa Mwananchi kwenda kumsikiliza, niombe sana Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) simamieni hilo, Serikali hii mmeiweka nyinyi sasa mkijifanya wadogo na kufanya Watendaji kuwa wakubwa mnakosea, wasimamieni Watendaji warudi wakasimamie Wananchi”
Amesema haivumiliki kero za wananchi kufika ngazi za juu wakati kuna viongozi katika kila ngazi.
“Haipendezi kuna wasimamizi wa shughuli za Wananchi ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata mpaka Vijiji lakini unapokea pale Ikulu kero ya Mwananchi wa Kijiji inakuja kule Ikulu, haipendezi, tuliowaweka kwenye ngazi hizo mna kazi gani!?, kaeni vizuri fanyeni kazi zenu vinginevyo hatutowavumilia kupokea tena kero za Wananchi kule Ikulu wakati huku kuna Viongozi wapo”
Mhe. Rais Samia amehitimisha ziara yake aliyoifanya katika mkoa wa mtwara kuanzia Septemba 14, hadi Septemba 17, 2023 ambapo amezindua miradi mbalimbali muhimu ikiwemo ya afya, maji, barabara na kuzungumza na wananchi katika maeneo yote.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.