Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano – Masasi Mji
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Elimu Ndugu Gerald Geofrey Mweli, ameridhishwa na uwekaji sawa wa miundo mbinu ya Shule ya Sekondari ya wasichana Masasi ikiwa ni maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajiwa kuanza masomo yao siku ya jumatatu ya tarehe 01/06/2020 ikiwa ni agizo lililotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli, la kufungua vyuo na Shule za Sekondari kwa wanafunzi wa Kidato cha sita.
Ndugu Mweli, ambaye ametembelea Shuleni hapo leo amewatoa hofu wazazi na walezi kutokana na mikakati thabiti iliyowekwa na Serikali yenye lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu katika mazingira yaliyo salama hasa kipindi hiki ambacho tahadhari kubwa inatakiwa kuchukuliwa kutokana na janga la ugonjwa wa COVID – 19.
“Wakurugenzi na Wakuu wa Shule, mnapaswa kuhakikisha ya kwamba wanafunzi wanajengwa kisaikolojia na kuwaondolea hofu ili waweze kuzingatia masomo na akili yao iweze kurudi katika hali ya kawaida” alisema Ndugu Mweli.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi Bi Gimbana Emmanuel Ntavyo amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu ya kwamba Halmashauri ya Mji Masasi imechukua tahadhari zote zilizotolewa na Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, na kwamba tayari Halmashauri imeandaa vifaa kinga vya kutosha ili wanafunzi hao waweze kujikinga na ugonjwa wa COVID – 19.
Kabla ya kutembelea Shuleni hapo, Naibu Katibu Mkuu na msafara wake ambao uliongozwa na Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara Bi Germana Mung’aho, walitembelea Shule ya Msingi ya mfano Kitunda iliyopo Kata ya Mkuti Halmashauri ya Mji Masasi ambapo Ndugu Mweli alipongeza jitihada zilizofanywa na Halmashauri ya Mji Masasi katika kusimamia ujenzi wa Shule hiyo pamoja na kutoa fedha shilingi milioni sitini na nane (68,000,000/=) kutoka kwenye mapato yake ya ndani ili kuongezea nguvu ujenzi wa shule hiyo.
Ndugu Mweli, amewataka Walimu wa Shule hiyo ya Msingi Kitunda kufanya kazi kwa bidii ili ubora wa miundo mbinu ya Shule hiyo uendane na ufaulu nzuri kwenye mithani ya Kitaifa.
Ndugu Gerald Geofrey Mweli (Kulia, mwenye koti) akielekea kweye Bwalo la chakula ili kuzungumza na Walimu wa Shule ya Msingi Kitunda
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.