Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano –Masasi Mji
Halmashauri ya Mji Masasi imepata pongezi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Gaspar Byakanwa kutokana na kupata hati safi ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ambao umeishia mwezi Juni 2019.
Mheshimiwa Byakanwa alitoa pongezi hizo leo kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kwa ajili ya kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG); Kikao ambacho kilifanyika katika ukumbi wa Saint Jordan Migongo Mission.
Mheshimiwa Selemani Mzee, Mkuu wa Wilaya ya Masasi akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ili aweze kuongea na Wajumbe wa Mkutano.
Katika ukaguzi huo wa hesabu za serikali kuanzia Julai mosi 2018 hadi mwezi Juni 2019, Halmashauri ya Mji Masasi ilikuwa na jumla ya hoja 20, ambapo kati ya hoja hizo, hoja 9 zilipatiwa majibu na kufungwa, wakati hoja 1 ilihamishiwa mamlaka ya maji vijijini (RUWASA), na hoja 10 zinaendelea kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Hamisi Ausi Mnela (Kisiki cha Mgomba), Diwani wa Kata ya Matawale, akichangia hoja wakati wa kuijadili taarifa ya CAG.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, mbali na pongezi hizo ameiagiza menejimenti ya Halmashauri ya Mji Masasi ihakikishe inaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vinatekelezeka ndani ya muda mfupi.
Mheshimiwa Byakanwa, alitumia nafasi hiyo pia, kutoa elimu juu ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19 kwamba ijapokuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamepungua kwa kiasi kikubwa, bado wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari zinazoelekezwa na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi kwa lengo la kumarisha kinga ya mwili.
Akifunga Mkutano huo maalum, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mheshimiwa Sospeter Nachunga, alitoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na msafara wake kwa ujumla kutokana na maelekezo na miongozo mizuri ambayo ameitoa kwenye mkutano huo, kwa kuwa yote yamelenga katika kuboresha ufanisi na kuinua maendeleo ya Halmashauri ya Mji Masasi.
Mheshimiwa Sospeter Nachunga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi akimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kabla ya kufunga Mkutano
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.