Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Gaspar Byakanwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Masasi na Halmashauri ya Wilaya Masasi (hawapo pichani)
Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Masasi Mji
“Tunapaswa kuondokana na upungufu wa vyoo, nimeamua kulibeba jukumu hili baada ya kugundua choo ni tatizo kwenye Shule zetu”, Kauli hiyo imetolewa Jumamosi tarehe 21/09/2019 na Mheshimiwa Gelasius Gaspar Byakanwa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alipokuwa akizungumza kwenye kikao kilichohusisha Wakuu wa Idara na vitengo, Waheshimiwa Madiwani, na Wakuu wa Taasisi mbalimbali zilizopo Wilayani Masasi.
katika kikao hicho Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliwahamasisha Wajumbe na wananchi wa Wilaya ya Masasi kwa ujumla kuchangia ujenzi wa vyoo bora vya Wanafunzi na Walimu kwenye Shule za Msingi na Sekondari ili kuyafanya mazingira ya kufundishia na kujifunzia kuwa rafiki kwa Walimu na Wanafunzi.
Akitoa takwimu za mahitaji ya matundu ya vyoo kwenye Shule zilizopo Mkoani Mtwara, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alisema, Matundu ya vyoo ambayo yanahitajika ni 6547 kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, wakati matundu 1830 yanahitajika kwa ajili ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari.
Kupitia harambee aliyoiendesha kwenye kikao hicho cha Watumishi, huku akisisitiza ya kwamba jukumu la ujenzi wa vyoo kwenye shule zilizopo Mkoani Mtwara ni la wana Mtwara wote, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alifanikiwa kupata ahadi ya kiasi cha Tsh.8,210,000/=, Saruji mifuko 27, na matundu manne ya vyoo ambapo hadi kufikia tarehe 10/10/2019 ahadi zitakuwa zimekamilishwa.
Aidha, Mheshimiwa Byakanwa aliwataka watumishi kushiriki vyema kwenye maandalizi na uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24/11/2019, “Kuanzia tarehe 8/10/2019 hadi tarehe 14/10/2019 Kutakuwa na zoezi la kuandikisha wapiga kura ambao ni wakazi wa eneo husika, Wananchi wenye sifa wahamasishwe kujiandikisha na kugombea nafasi mbalimbali.” Alisisitiza Mheshimiwa Byakanwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, alitumia kikao hicho kuwafunda Watumishi na Madiwani wa Halmashauri zote mbili kuona umuhimu katika suala zima la kuwekeza. Alisema kutowekeza kunasababisha kupungua kwa wigo wa ajira kwa sababu wenye fursa ya kuwekeza hawafanyi hivyo.
Mheshimiwa Byakanwa, akiwa Wilayani Masasi jana Jumamosi amefanya vikao vitatu tofauti kwa lengo la kuhamasisha Wadau na wananchi Wilayani humo kuchangia ujenzi wa vyoo vya Walimu na Wanafunzi chini ya Kampeni aliyoiasisi ya “SHULE NI CHOO.” Pamoja na Kuhamasisha ushiriki wa Wananchi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chini ya kauli mbiu isemayo “Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa ni Chachu ya Mendeleo, ni Haki na Wajibu Wako Kujiandikisha, Kugombea, na Kuchagua Kiongozi Bora.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.