Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mheshimiwa Selemani Mzee amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali Wilayani humo kuwakemea watu wote ambao watajitokeza kwa wananchi na kuanza kufanya kampeni kabla ya muda.
Mheshimiwa Selemani Mzee amesema kufanya kampeni kabla ya vikao rasmi ndani ya chama husika kufanyika ni kusababisha vurugu kwa wananchi. Alisisitiza ya kwamba Wilaya ya Masasi haipo tayari kuruhusu vurugu ambazo zitasimamisha shughuli za maendeleo.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa agizo hilo leo baada ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwenye Ofisi ya Mtaa wa Wapiwapi A, Kata ya Napupa, Halmashauri ya Mji Masasi.
Akizungumzia zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Mheshimiwa Selemani Mzee amewataka Wananchi wa Wilaya ya Masasi ambao wana umri wa miaka 18 na kuendelea na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiandikisha na kupata vitambulisho vitakavyowawezesha kupiga kura.
Alisisitiza ya kwamba zoezi hilo pia ni fursa kwa kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka Kata moja kwenda nyingine, Jimbo moja kwenda jingine n.k. Lakini pia kwa waliopoteza vitambulisho vyao au kuharibika, ni wakati muafaka kwao kupata vitambulisho vipya.
Zoezi la Kujiandikisha/kuboresha daftari la wapiga kura kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara limeanza jana Jumapili tarehe 12/01/2020 na litakamilika Jumamosi ya tarehe 18/01/2020.
Kwa mujibu wa Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Masasi Mjini Ndugu Gresha Sanga, jana ambayo ni siku ya kwanza ya zoezi hilo jumla ya watu 2961 wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, wakati watu 1667 wameboresha taarifa zao na kupatiwa vitambulisho vipya baada ya kubadilisha makazi yao, na watu 12 wamefutiwa taarifa zao kutokana na kukosa sifa ikiwa ni pamoja na kufariki.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.