Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Halmashauri ya Mji Masasi Masasi "Imeifungua" Masasi Mji na kuleta "Nuru" kwa watoto, wakina mama, vijana, wazee, wakulima, wafugaji, wagonjwa na wananchi wote wa Masasi.
Shamrashamra zilianza mapema Septemba 9, 2023 mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed kutangaza ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba Septemba 14 hadi Septemba 17, 2023 mchana na usiku atahamia mkoani humo.
Ilikuwa ni habari mpya, kubwa na yenye msisimuko kwa wananchi wa Mtwara. Hatimaye Septemba 14, 2023 Mhe. Rais Samia aliwasili rasmi Mtwara na kupokelewa na maelfu ya wananchi wa mkoa huo.
Ujio huo ulizidi kuenea na kusambaa kwa kasi baada ya ratiba ya Mhe. Rais Samia kuonesha atatembelea Masasi Mji.
Maarufu kama "Kariakoo" ya Mtwara kama alivyobainisha Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauter John Kanoni wakati akiwatambulisha viongozi akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mhe. Hashim Namtumba sambamba na Mkurugenzi wa Mji Masasi Bi. Erica Yegella kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa Rais Dkt Samia uliofanyika katika uwanja wa boma Masasi mjini Septemba 17, 2023.
"Mji huu wa Masasi ni mji wa kibiashara, hapa ni katikati ya maeneo yote, halmashauri zote zinakuja kutafuta mahitaji yao hapa, kariakoo yao ni hapa" anasema Mhe Kanoni.
Mji huu upo kilomita 210 kusini magharibi mwa mkoa wa Mtwara, ukiwa na ukubwa wa hekta 37,920 huku idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi 2022 ikiwa ni watu 137,585 wanaume wakiwa 65,781 na wanawake 71,804 wakiupamba Mji kwa shughuli za kilimo cha Korosho, ufuta, mbaazi na mazao mbalimbali ya chakula.
Mji huu unafikika kwa urahisi kutoka pande zote za nchi kwani ni makutano makuu ya barabara kuu ya Tunduru-Songea- Lindi-Dar es salaam-Mbeya, Nachingwea-Liwale-Newala- Tandahimba ukipambwa na hoteli za kifahari, masoko ya bidhaa, viwanda na viwanja vya uwekezaji.
Lakini pia, mtandao wa barabara umeimarishwa kama anavyobainisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuwa mtandao wa barabara unaongezwa kutoka kilometa 6.9 hadi kilometa 11.2.
" Wana masasi wanakushukuru sana Mhe. Rais kwa kazi hii ya kuongeza mtandao wa barabara na kuongeza taa za barabarani" anasema Mhe. Mchengerwa.
Lakini pia, Nuru kwenye sekta ya afya imepatikana kama alivyobainisha Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini, Mhe. Geoffrey Mwambe wakati akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Masasi.
"Mhe.Rais nakushukuru sana kwa kung'arisha Masasi, Mji unang'aa Mji ni mpya barabara za lami ziko nyingi na zinapendeza na upande wa afya zaidi ya shilingi bilioni 2 umetuletea wanamasasi kwa ajili ya ukarabati wa hospitali yetu ya wilaya Mkomaindo hadi kufikia 2025 hospitali yetu itakuwa mpya"
Aidha, Nuru ikapatikana kwenye sekta ya maji ambapo Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema Serikali itatoa fedha kiasi cha Tsh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa chanzo cha maji Nangowo ili maji safi ya uhakika na kutosha yapatikane Masasi na maeneo ya pembezoni.
Hatimaye, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan akahutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo.
"Nawashukuru sana wananchi wa Masasi kwa kujitokeza kwa wingi namna hii, nashukuru kwa heshima mliyonipa"
Ujio wake katika Halmashauri ya Mji Masasi Masasi "Umeifungua" Masasi Mji na kuleta "Nuru" kwa watoto, wakina mama, vijana, wazee, wakulima, wafugaji, wagonjwa na wananchi wote wa Masasi.
Nuru kwenye "Umeme" Mhe.Rais Samia amesema safari ya kuondoa adha ya kukatika kwa umeme ndani ya Masasi imeanza na Serikali imejizatiti katika hilo.
" Kwa sasa mkandarasi yupo kazini kuinganisha Masasi kwenye Gridi ya Taifa kutokea Ruvuma. Pia kuna mkandarasi anatoa umeme Ruangwa kupitia Nangugwa, ambao utakuwa tayari ifikapo Desemba mwaka huu. Baada ya miezi 18 umeme wa uhakika utakuwa umefika".
Nuru kwenye "Kilimo" mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta mafanikio kwenye zao la mbaazi, wananchi wamepata ongezeko la thamani ya zao hilo lakini pia kuhusu korosho Mhe. Rais amesema Serikali inajenga kongani ya viwanda ili kuongeza thamani ya zao hilo.
"Suluhisho la kupata bei nzuri ya korosho ni kuongeza thamani korosho zetu. Katika kuongeza thamani tunajenga kongani ya viwanda, Maranje ambapo patakuwa na kituo cha kukoboa korosho zote za Mtwara. Korosho zitaongezwa thamani, ili tuuze korosho zilizotengenezwa.Tukiongeza thamani bei itakuwa nzuri".
Aidha akawakumbusha wananchi wa Masasi kutumia fedha kwenye mambo yenye tija sambamba na kusisitiza suala la elimu kwa kupunguza tamaduni zinazochochea ongezeko la mimba utotoni.
"Wachezeni wakiwa na umri mkubwa huku wakijua mambo wanayofundishwa" Mhe. Rais Dkt. Samia
Kazi iendelee " Nataka niwaambie ndugu zangu wa Masasi kwamba, Maendeleo yanakuja kwa vitendo na kwakuchukua hatua mahususi na si kwa maneno. Maendeleo ni vitendo. Ninatoa rai kwa watanzania wote popote walipo kuunga mkono jitihada hizi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii. Kama ni mkulima anza sasa kuongeza mashamba, ili mazao yawe mengi zaidi, kwani Serikali imejitoa kukuza kilimo kwa kiasi kikubwa",
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihitimisha ziara yake Mkoani Mtwara katika viwanja vya Boma, Halmashauri ya Mji Masasi.
Karibu Halmashauri ya Mji Masasi, Viwanja vya Biashara, Makazi na Uwekezaji vinapatikana, Karibu uwekeze Masasi.
Imetolewa na,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Halmashauri ya Mji Masasi.
Septemba 19, 2023.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.