Na Kitengo cha Habari na Mawasiliano – Masasi Mji
Wataalamu kutoka Idara ya Afya Halmashauri ya Mji Masasi wameendesha mafunzo kwa Wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi leo hii ili kuwapa muongozo uliotolewa na Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya vyuo na taasisi nyingine za kielimu juu ya kujikinga na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Wataalamu hao ambao waliongozwa na Mratibu wa Huduma za afya Shuleni Bi Theresia Moyo, walijikita kutoa Elimu kwa wanafunzi hao zaidi ya 150 juu ya namna ya uvaaji sahihi wa barakoa, unawaji wa mikono kwa kutumia maji yanayotiririka na matumizi ya vitakasa mikono mara kwa mara.
Wanachuo hao ambao wamefungua Chuo leo hii ikiwa ni agizo lililotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli, la kufungua vyuo na shule za sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha sita.
Baadhi ya Wanachuo wa Chuo cha Maendeleo Masasi (FDC) wakifuatilia kwa makni mafunzo kutoka kwa Wataalamu wa afya (Hawapo pichani).
Akitoa neno la Shukrani kwa wataalamu hao, Mkuu wa Chuo hicho Ndugu Halfan Bashiri Mshana aliwashukuru wataalamu hao kwa kutenga muda na kufika chuoni hapo ili kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanachuo hao ambao ndio kwanza wamerejea chuoni hapo kutoka kwao.
Alitumia fursa hiyo kuwajulisha wanachuo hao ya kwamba ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19, yapo mabadiliko kadhaa ambayo watayaona chuoni hapo ikiwa ni pamoja na upokeaji wa chakula kwa awamu kufuatana na ratiba ambayo imeandaliwa, ulalaji ambapo ili kupunguza msongamano mabwenini vipo vyumba vya madarasa kadhaa ambavyo vitageuzwa kuwa mabweni, lakini pia upo utaratibu mpya wa kupata masomo kwa awamu ambako kutasababisha vipindi kuishia saa 11 jioni badala ya utaratibu ambao wanachuo hao wameuzoea wa vipindi vya kuisha saa 8 na nusu mchana.
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.