Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Masasi limepitisha bajeti ya shilingi 24,015,608,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha ujao 2023/2024, Bajeti hiyo imejadiliwa na kupitishwa na Waheshimiwa Madiwani katika Mkutano Maalum wa Baraza la Halmashauri ya Mji Masasi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Hashimu Hashimu Namtumba Kweka, ameliongoza Baraza hilo kwa kuwapitisha Waheshimwa Madiwani kujadili Mapendekezo ya Makisio ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Waheshimiwa Madiwani wameipitia Mpango na Bajeti hiyo kipengele kwa kipengele na kisha kuipitisha kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa mwaka wa fedha ujao 2023/2024.
Mwenyekiti Halmashauri ya Mji Masasi Mhe. Namtumba amesema anaamini bajeti hiyo ambayo imepitishwa kwaajili ya utekelezaji wake kwa mwaka ujao wa fedha, itakidhi matakwa ya Halmashauri kwakuwa imekuwa bajeti iliyoelekezwa zaidi kwenye vipaumbele vya Halmashauri. “Tuna imani kubwa na bajeti hii kwa maana imeandaliwa vyema tofauti , hivyo ikitekelezwa katika uhalisia wake tutafikia malengo ya vipaumbele tulivyojiwekea”, aliongeza Namtumba.
Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi, Elias Ntiruhungwa amesema kuwa utekelezaji wa bajeti unategemea na upatikanaji wa fedha, na anamini bila shaka bajeti iliyopitishwa na baraza la madiwani itasimamiwa vyema ili kutekeleza yale yote yaliyopendekezwa. “Tutasimamia vyema utekelezaji wa bajeti iliyopitisha, ili kuhakikisha vipaumbele vilivyobainishwa ikiwemo miradi ya maendeleo inatekelezwa”, alisema Ntiruhungwa.
Aidha, Ntiruhungwa amesema kuwa miradi mbalimbali na vipaumbele vilivyobainishwa itatekelezwa kwa wakati kwa kusimamia vyema mapato ya ndani ili kutekeleza miradi mbalimbali inayotokana na fedha za mapato ya ndani. “Tutaimarisha vikosi kazi, na mbinu mpya zitakazoongeza mapato ya Halmashauri kwa kiasi kikubwa ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti hii”, Ntiruhungwa .
Madiwani wamesema kuwa bajeti hii ina maono mazuri kwani imeainisha maeneo muhimu ambayo yataleta chachu kubwa ya Maendeleo ya Halmashauri ya Mji Masasi, Miongoni mwa vipaumbele vilivyobainishwa ni pamoja na utengenezaji wa miundombinu katika taasisi zikiwemo shule, Zahanati na vituo vya afya, Maeneo mengine ni pamoja ya kuimarisha ustawi wa jamii kwa kutoa Mikopo ya asilimia 10 ya Mapato ya ndani kwa Vijana ,Wanawake na walemavu.
Bajeti ya Halmashauri ya Mji Masasi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imekisia kukusanya na kupokea jumla ya Shilingi 24,015,608,000.00 kati ya fedha hizo Mapato ya Ndani ni Shilingi 2,855,980,500.00 Ruzuku na Matumizi ya kawaida na Mishahara ni Shilingi 15,737,987,000 na Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 8,277,621,400.00 .
MASASI TOWN COUNCIL
Anuani ya Posta: P.O BOX 447 MASASI
Simu Ya Mezani: +255 23 2510685
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: info@masasitc.go.tz
Haki Miliki@ Halmashauri ya Mji Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa.